MWANZO
WA AGIZO LA KUSHIKA SABATO NA SABABU ZAKE
Kabla ya kujifunza kwa undani sana, juu ya mwanzo wa agizo
la kushika sabato na sababu zake, kwanza ni vema tukajifunza nini maana halisi
ya neno Sabato. Neno ‘Sabato’ ambalo
kwa kiingereza ni ‘Sabbath’
linatokana na neno la Kiebrania ‘Shabbath’
likiwa na maana ya ‘Pumziko’ au ‘kustarehe na kuacha kazi.’ Kwa Kiyunani
huitwa ‘Sabbaton.’ Na neno hili halimaanishi
siku ya kuabudu, bali ni pumziko la kazi.
Asili ya
sabato yaani pumziko la kazi, inapatikana katika kitabu cha Mwanzo, pale Mungu
alipomaliza kazi yake ya uumbaji na kupumzika siku ya saba (Mwanzo 2:1-3). Pamoja na Mungu
kupumzika siku ya saba, lakini bado Biblia haituambii kama Mungu aliwaagiza
Adam na Hawa kupumzika siku ya saba. Kadhalika maandiko hayatuoneshi kama Nuhu,
Ibrahimu, Isaka na Yakobo walifundishwa juu ya sheria ya kupumzika siku ya saba (sabato).
Agizo la kwanza kwa wanadamu, la kushika
sheria ya kushika siku ya sabato, lilitolewa na Mungu mwenyewe kwa Wana wa
Israeli tu, na kwa mkono wa Musa. Ni dhahiri kabisa, hata Israeli mwenyewe
yaani Yakobo, wakati akiwa hai, hakuwahi kusikia habari ya kupumzika siku ya
saba (sabato). Agizo hili halikutolewa kwa mataifa mengine, bali kwa wana wa
Israeli tu, na sababu kuu ni kwamba, kwa kipindi hicho, ni wana wa Israeli peke
yao ndiyo waliokuwa wanamjua Mungu wa kweli yaani Yehova. Ni kwa sababu hiyo
basi, Mungu aliwapa sheria (Torati) watu wake, yaani Amri kumi, sheria nyingine 613 na Hukumu zake. Katika kitabu cha Kumbukumbu la Torati 4:7-8 Biblia
inasema, “Kwa maana liko taifa gani
kubwa, lililo na Mungu aliye karibu nao, kama Bwana, Mungu wetu, alivyo, kila
tumwitapo? Tena liko taifa gani kubwa, lililo na amri na hukumu zenye haki
kama torati hii yote, ninayoiweka mbele yenu leo.” Lakini pia Musa mwenyewe alithibisha kwamba,
sheria ya kushika siku ya sabato na sheria nyingine haikuanza na baba zao, bali
ilianza na wao wenyewe yaani wana wa Israeli; katika Kumbukumbu la torati 5:1-3 Biblia inasema, “Musa akawaita Israeli wote, akawaambia, Enyi Israeli, zisikieni amri na
hukumu ninenazo masikioni mwenu leo, mpate kujifunza na kuangalia kuzitenda.
Bwana Mungu wetu, alifanya agano nasi katika Horebu. Bwana hakufanya agano hili
na baba zetu, bali na sisi, yaani sisi sote tulio hapa, tu hai.” Wapo baadhi ya washika sheria ya siku ya
sabato wa nyakati za leo, ambao hutoa madai ya kwamba, Adamu alikuwa ni msabato
wa kwanza. Kigezo wanachotumia, ni kwa sababu Mungu alipumzika siku ya saba, hivyo
husema kwamba, Adamu naye alipumzika ingawa Biblia haituambii kama Adamu
alipumzika. Na kama alipumzika, alipumzika kwa sababu ya kazi ipi aliyoifanya?
Maana kazi ya uumbaji ilifanywa na Mungu peke yake. Musa ambaye ndiye aliyekuwa
msabato halisi, anaipinga hoja hii katika mistari tuliyosoma hapo juu kwa
kusema kwamba, Mungu hakufanya agano la zile sheria na baba zao, bali wao
wenyewe. Kwa hiyo ni wazi kabisa, kuanzia Adamu mpaka Yakobo hawakuwahi
kuambiwa na Mungu juu ya sheria ya kushika siku ya sabato.
SABABU ZILIZOPELEKEA WANA WA ISRAEL KUPEWA
SHERIA YA KUSHIKA SABATO
Ziko
sababu kuu mbili zilizopelekea wana wa Israeli peke yao, kuamriwa kushika
sabato;
1.
NI
KUMBUKUMBU KWA WANA WA ISRAELI KUWA WALIKUWA WATUMWA KATIKA NCHI YA MISRI.
Katika
kitabu cha Kumbukumbu la torati 5:15
Biblia inasema, “Nawe utakumbuka ya kuwa
wewe ulikuwa mtumwa katika nchi ya Misri, na ya kuwa Bwana, Mungu wako,
alikutoa huko kwa mkono wenye nguvu, na mkono ulionyoshwa, kwa sababu hiyo
Bwana, Mungu wako, alikuamuru ushike sabato.’’ Kwa hiyo, ni wana
wa Israeli peke yao, ndiyo walio amriwa kushika sheria ya siku maalum ya
kupumzika yaani sabato, ili kwao iwe kumbukumbu kwamba, walikuwa watumwa katika
nchi ya Misri. Kwa hiyo, kwa mtu asiye Mwana wa Israeli akishika sheria ya siku
ya sabato, atakuwa anakumbuka nini? Je alishawahi kuwa mtumwa huko Misri?
2.
WANA WA
ISRAELI WALIAMRIWA KUISHIKA SABATO ILI IPATE KUWA ISHARA YA AGANO KATI YAO NA
MUNGU.
Katika
kitabu cha Kutoka 31:13 Biblia
inasema, “Kisha, nena wewe na wana wa
Israeli, na kuwaambia, Hakika mtazishika sabato zangu, kwa kuwa ni ISHARA
kati ya mimi na ninyi, katika vizazi vyenu vyote, ili mpate kujua ya kuwa mimi
ndimi Bwana niwatakasAye ninyi.” Kadhalika katika kitabu cha Kutoka 31:16-17 Biblia inasema, “Kwa ajili ya hayo wana wa Israeli
wataishika sabato, kuiangalia sana hiyo, katika vizazi vyao vyote, ni agano la
milele. Ni ISHARA kati ya mimi na wana wa Israeli milele…..” Pia
katika Ezekieli 20:20 Neno la Mungu
linasema, “Zitakaseni sabato zangu, nazo
zitakuwa ISHARA kati ya mimi na ninyi, mpate kujua ya kuwa mimi ndimi
Bwana, Mungu wenu.” Ezekiel 20:12
inasema, “Tena naliwapa sabato zangu,
ziwe ISHARA kati yangu mimi na wao…..”
ANGALIZO: Neno ishara linamaanisha siyo kitu halisi,
bali ni kitu kinacho ashiria kitu fulani ambacho kitakuja, ni kitu
kinachoelekeza kitu fulani halisi ambacho kitakachokuja. Sabato ilikuwa
ikiashiria pumziko halisi ambalo Bwana Yesu amekuja kuwapa watu duniani, na
ndiyo sababu ya Yeye kujiita Bwana wa pumziko (sabato) (Luka 6:5) akimaanisha kuwa Yeye ndiye mtoa pumziko. Roho Mtakatifu kupitia Mtume Paulo, amefafanua
katika kitabu cha Wakolosai kuwa, sabato ilikuwa ni kivuli cha mambo yajayo.
Sabato ilikuwa siyo kitu halisi na ndiyo maana mtu akisha pata kitu halisi
hawezi tena kung’ang’ania ishara au kivuli (negative). Wakolosai 2:16-17 inasema, “Basi,
mtu asiwahaukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au
mwandamo wa mwezi, au SABATO; mambo hayo ni kivuli cha mambo yajayo;
bali mwili ni wa Kristo.”
IDADI
YA SABATO AMBAZO WANA WA ISRAELI WALIAMRIWA
KUZISHIKA
NA MALENGO YAKE
Katika kushika
sheria ya sabato, Wana wa Israeli hawakupewa sabato moja tu, yaani sabato ya
siku, kama wanavyofanya wanaojiita wasabato wa leo. Kwa mtu mwenye ufahamu
sahihi wa maandiko, anaweza akahoji maswali mengi, na ya msingi sana dhidi ya
wanaoshika sabato katika nyakati za leo. Kabla hatujaingia kwa undani zaidi,
ebu tuangalie idadi ya sabato ambazo wana wa Israeli waliamriwa kuzishika.
Katika kitabu cha Walawi 26:2 Neno
la Mungu linasema, “Zishikeni SABATO
ZANGU, na kupastahi patakatifu pangu; mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.”
Tunaona hapa Mungu anatumia neno ‘sabato
zangu’ na siyo ‘sabato yangu’. Tukiangalia katika Ezekieli 20:20 Biblia inasema, “Zitakaseni SABATO ZANGU; nazo zitakuwa ishara kati ya mimi na
ninyi, mpate kujua ya kuwa mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.” Tunaona na hapa
Mungu anatumia ‘sabato zangu’ na
siyo ‘sabato yangu’. Katika kitabu cha Kutoka
31:13 inasema, “Kisha, nena wewe na
wana wa Israeli, na kuwaambia, Hakika mtazishika SABATO ZANGU, kwa kuwa
ni ISHARA kati ya mimi na ninyi, katika vizazi vyenu vyote, ili mpate kujua ya
kuwa mimi ndimi Bwana niwatakasaye ninyi.” Kadhalika na hapa Mungu anatumia
neno ‘sabato zangu’ na siyo ‘sabato
yangu’. Pia katika kitabu cha Walawi
19:30 Biblia inasema, “Zishikeni SABATO
ZANGU, mpaheshimu patakatifu pangu; mimi ndimi Bwana.” Na hapa pia
tunaona Mungu anatumia neno ‘sabato
zangu’ na siyo ‘sabato yangu’. Kwa hiyo, hii inatuthibitishia wazi kabisa
kwamba, Mungu hakuawaagiza wana wa Israeli kushika sabato moja ya siku kama
wanavyofanya wanaojiita wasabato wa leo.
IDADI
YA SABATO ZILIZOAMRIWA NA MUNGU ILI
WANA WA
ISRAELI WAZISHIKE
Kulingana
na maandiko, wana wa Israeli walipewa sabato zaidi ya moja, zifuatazo ni baadhi
ya sabato hizo;
1.
SABATO
YA SIKU.
Sabato
ya siku ni pumziko ambalo lilifanywa baada ya siku sita za kazi, hivyo siku ya
saba, walipewa amri ya kupumzika, kama tunavyoweza kuiona katika amri ya nne miongoni
mwa amri kumi. Katika kitabu cha Kutoka
35:2 Biblia inasema, “Fanyeni kazi siku sita, lakini siku ya saba
itakuwa siku takatifu kwenu; ni sabato ya kustarehe kabisa kwa Bwana, mtu awaye
yote atakayefanya kazi yoyote katika siku atauawa.” (Soma pia Kutoka 31:14-15; Kumbukumbu 5:14).
2.
SABATO
YA MWAKA.
Sabato
ya mwaka ni pumziko ambalo lilifanywa baada ya miaka sita ya kazi, hivyo mwaka wa
saba, wana wa Israeli walipewa amri ya kupumzika mwaka mzima. Tunaweza kuona
sabato hii katika kitabu cha Walawi
25:1-5, “Kisha Bwana akanena na Musa
katika mlima wa Sinai, na kumwambia. Nena na wana wa Israeli, hapo mtakapoingia
katika nchi niwapayo, ndipo hiyo nchi itashika sabato kwa ajili ya Bwana. Panda
shamba lako miaka sita, na miaka sita lipalie shamba lako la mizabibu, na
kuyachuma matunda yake; lakini katika mwaka wa saba itakuwa ni sabato ya
kustarehe kwa ajili ya hiyo nchi, ni sabato kwa Bwana; usipande shamba lako
wala usipalie shamba lako la mizabibu. Hicho kimeacho chenyewe katika mavuno
yako, usikivune, wala zabibu za mizabibu isiyopelewa usizitunde, UTAKUWA
MWAKA WA KUSTAREHE KABISA KWA AJILI YA NCHI HIYO. Na hiyo sabato ya nchi
itakuwa chakula kwenu; kwako wewe, na
kwa mtumwa wako, na kwa mjakazi wako, na kwa mtumishi aliyeajiriwa, na kwa
mgeni wako akaaye pamoja nawe.”
3.
SABATO
YA SABATO SABA ZA MIAKA (YUBILEE)
Sabato
hii ni pumziko ambalo lilifanywa baada ya sabato saba za miaka yaani miaka saba
mara saba unapata miaka 49, hivyo mwaka wa hamsini, wana wa Israeli waliamriwa
kupumzika. Kwa jina lingine iliitwa Yubile. Sabato hii tunaweza kuiona katika
kitabu cha Walawi 25:8-11, “Nawe utajihesabia sabato saba za miaka,
maana, miaka saba mara saba; zitakuwa ni siku za sabato saba za miaka kwenu,
maana miaka arobaini na kenda (49).Ndipo utakapoipeleka pande zote hiyo
baragumu, yenye sauti kuu, siku ya kumi ya mwezi wa saba; katika siku hiyo ya
upatanisho mtaipeleka baragumu katika nchi yenu yote. NA MWAKA WA HAMSINI
MTAUTAKASA, na kupigwa mbiu ya kuachwa mahuru katika nchi yote kwa watu wote
waiketio, itakuwa ni yubile kwenu; nanyi kila mtu atairudia milki yake
mwenyewe, nanyi mtarejea kila mtu kwa jamaa yake. Mwaka huo wa hamsini utakuwa
ni yubile kwenu; MSIPANDE MBEGU, WALA MSIVUNE, KITU HICHO KIMEACHO CHENYEWE,
WALA MSIZITUNDE ZABIBU YA MIZABIBU ISIYOPELEWA.”
Ebu mtoto wa Mungu
sasa tujiulize swali, kama kweli wasabato wa leo wako sahihi kushika sabato, kwa
nini wanashika sabato ya siku peke yake? Je mbona hizi nyingine zimewashinda? Kama
sabato inayoshikwa leo na wasabato, msingi wake ni Biblia, mbona hizi sabato
nyingine wameziacha na wakati zote ziliamriwa na Mungu mwenyewe? Hata hivyo
Neno la Mungu katika kitabu cha Yakobo
2:10 inasema, “Maana mtu awaye yote
atakaye ishika sheria yote, ila akajikwaa katika neno moja, amekosa juu ya
yote.” Kwa hiyo kama wasabato wa leo wanashika sabato ya siku tu, na kuacha
sabato nyinginezo, ni wazi kabisa wamekosa juu ya yote.
MALENGO
YA KUSHIKA SABATO KWA WANA WA ISRAELI
Lengo la kushika sabato kwa
wana wa Israeli lilikuwa ni kupumzika kazi na kustarehe tu na wala si
vinginevyo. Wanaojiita wasabato katika nyakati za leo, wameigeuza sheria hii ya
kushika sabato kama ni siku ambayo Mungu ameamuru wafanye ibada, kinyume kabisa
na kusudi zima na maana halisi ya neno sabato. Watu hawa wamekuwa wakishutumu
wakristo wengine na kusema kuwa, Jumamosi ndiyo siku halali ya kufanya ibada,
lakini Jumapili, ni siku ambayo haikuamriwa na Mungu, watu kukusanyika kufanya
ibada. Ni vema ifahamike kuwa agizo la kushika sabato na siku ya kukusanyika ni
vitu viwili tofauti na ni maagizo mawili tofauti ambayo wana wa Israeli
walipewa kuyatekeleza. Katika agizo la kukusanyika kwa wana wa Israeli, Mungu
alitoa siku mbili yaani Jumapili na
Jumamosi, ingawa wasabato karibu wote hawalijui jambo hili, maana hao wamekaririshwa
siku ya sabato tu yaani Jumamosi. Tunaweza kuthibitisha ukweli huu katika
kitabu cha Kutoka 12:16 Biblia
inasema, “SIKU YA KWANZA kutakuwa
kwenu na kusanyiko takatifu, na SIKU YA SABA kutakuwa na kusanyiko
takatifu, haitafanywa kazi yoyote katika SIKU HIZO, isipokuwa kwa hiyo
ambayo kila mtu hana budi kula, hiyo tu ifanyike kwenu.” Mungu aliwaamuru
wana wa Israeli wakusanyike siku ya
kwanza ya juma yaani Jumapili na
siku ya saba yaani Jumamosi kwa kalenda ya kwetu. Pia
Mungu hakuwaagiza kukusanyika tu, bali aliwaagiza wasifanye kazi pia. Lakini
wanaojiita wasabato nyakati za leo, wanapinga kukusanyika Jumapili sawasawa na
maagizo ya torati wanayodai kuifuata. Swali ni kwamba, mafundisho yao ya
kukusanyika siku ya sabato yametoka wapi? Kama ni kwenye Biblia mbona siku moja
hii wameiacha? Je aliyetoa agizo la siku ya sabato ni Mungu mwingine na
aliyetoa agizo katika kitabu cha Kutoka
12:16 (yaani kukusanyka siku ya Jumapili) ni Mungu mwingine?
Kwa hiyo agizo la
kukusanyika lilikuwa ni siku mbili, imetajwa ya kwanza ni Jumapili (siku ya
kwanza ya juma) na ya pili ni Jumamosi (siku ya saba) kwa kalenda yetu, kama
tulivyoona katika kitabu cha Kutoka
12:16. Sasa tukija kwenye agizo la kushika sabato halikuwa ni siku ya
kukusanayika, bali ni pumziko la kazi tu na kustarehe kama tunavyoweza kuona
katika kitabu cha Kutoka 31:14-15, “Basi mtaishika hiyo sabato; kwa kuwa ni
takatifu kwenu; kila mtu atakayeitia unajisi hakika yake atauawa; kwa kuwa kila
mtu afanyaye kazi siku hiyo, nafsi hiyo itakatiliwa mbali na watu wake.
Kazi itafanywa siku sita; lakini siku ya saba ni sabato ya kustarehe kabisa,
takatifu kwa Bwana, kila mtu atakayefanya kazi yoyote katika siku ya
sabato, hakika yake atauawa.” Mungu hapa anasema kila mtu atakayefanya kazi
siku hiyo atauawa, hajasema kila mtu atakaye kosa kwenda kwenye kusanyiko
atauawa. Na ndiyo maana kwenye Biblia, inapotaja neno sabato ina maana ya
kupumzika kazi na siyo kufanya kusanyiko la kuabudu kama wafanyavyo wanaojiita
wasabato wa leo. Pia Kutoka 35:2
Biblia inasema, “Fanyeni kazi siku sita,
lakini siku ya saba itakuwa siku takatifu kwenu; ni sabato ya kustarehe kabisa
kwa Bwana; mtu awaye yote atakayefanya kazi yoyote katika siku hiyo atauawa.”
Tunaona tena hapa, Mungu anasisitiza kwamba, atakayeuawa, ni yule atakayefanya
kazi siku ya sabato, na hakusema atakayekosa kwenda kukusanyika kwa ajili ya
ibada, kwani agizo hili lilihusiana na kupumzika kufanya tu. Kimsingi unaposema
sabato, siyo dhehebu, wala siyo siku ya kuabudu, bali ni pumziko la kazi.
Nyakati za leo, wanaojiita wasabato, wanachanganya siku ya kusanyiko na siku ya
pumziko la kazi. Tukiangalia tena maandiko katika kitabu cha Kumbukumbu la torati 5:14 kwenye ile
amri ya nne ya kushika sabato, Biblia inasema, “Lakini siku ya saba ni sabato ya Bwana, Mungu wako; siku hiyo usifanye
kazi yoyote, wewe, wala mwanao, wala binti yako, wala mtumwa wako, wala
mjakazi wako, wala ng’ombe wako, wala punda wako, wala mnyama wako yeyote, wala
mgeni aliye ndani ya malango yako, ili mtumwa wako na mjakazi wako wapumzike
vile vile kama wewe.” Kadhalika na hapa Mungu anaifafanua kwa uzuri kabisa,
maana ya sabato na lengo lake. Lengo lilikuwa watu wapumzike, wanyama
wapumzike, wafanyakazi wapumzike na kustarehe, kwa sababu hiyo, sabato
iliwagusa mpaka wanyama. Kama ingekuwa kwamba sabato ilimaanisha siku ya
kuabudu basi wanyama wasingetajwa kupumzika.
Mtu aliyepigwa mawe
hata kufa nyakati za Musa jangwani, hakuuawa kwa sababu hakwenda kuabudu siku
ya sabato, bali aliuawa kwa sababu alifanya kazi (Hesabu 15:32-36). Hii inathibitisha kwamba agizo la kushika sabato
lililenga pumziko la kazi tu na si agizo la kukusanyika kama wanavyodai
wasabato wa leo. Wana wa Israeli walikusanyika siku ya saba (Jumamosi) na siku
ya kwanza ya juma (Jumapili) kwa agizo la Mungu mwenyewe katika Kutoka 12:16, kama tulivyokwisha kuona
hapo nyuma. Kimsingi ni kwamba, katika amri kumi (Kumbukumbu 5:12-15), amri ya nne inazungumzia kupumzika kazi tu. Na
Kutoka 12:16 Mungu anatoa mwongozo
wa siku za kukusanyika kwa ibada. Swali ni kwamba, wasabato wa leo
wanakusanyika Jumamosi kwa msingi wa andiko lipi kati ya hayo? Kama kwa msingi
wa amri ya nne ya kushika sabato (Kumbukumbu
5:12-15), basi watakuwa wamepotea, maana pale haikuzungumziwa siku ya
kukusanyika kwa ajili ya ibada, bali ni pumziko la kazi tu. Lakini kama wana
kusanyika Jumamosi, kwa msingi wa andiko la Kutoka 12:16, kadhalika watakuwa wamepotea, maana, katika siku za
kukusanyika, katika andiko hili, Mungu ametoa siku mbili yaani siku ya kwanza
ya juma (Jumapili) na siku ya saba ya juma (Jumamosi), sasa mbona siku ya
kwanza ya Juma (Jumapili) wanaipinga? Ni wazi kabisa wanampinga Mungu.
ANGALIZO:
Ili
kupata pumziko vizuri siku ya sabato, wana wa Israeli waliagizwa na Mungu,
wasitoke mahali pao; Kutoka 16:29
Biblia inasema, “Angalieni, kwa kuwa
BWANA amewapa ninyi hiyo sabato, kwa sababu hii huwapa siku ya sita chakula cha
siku mbili; kaeni kila mtu mahali pake, mtu awaye yote asiondoke mahali pake
kwa siku ya saba. Basi hao watu wakapumzika siku ya saba.” Kwa hiyo,
nyakati zile, ilikuwa ni sheria kwa wana wa Israeli, kutotembea mwendo mrefu
siku ya sabato. Walitembea mahali pafupi sana, na hatimaye urefu ule wakauita
mwendo wa sabato (Matendo 1:12).
Wanaojiita wasabato wa leo, siku ya Jumamosi, wanatembea mwendo zaidi ya kilometa
moja, kwenda kanisani, je hii ni kweli sabato ya kweli (pumziko la kweli)?
HOJA ZA
WASABATO DHIDI YA WAKRISTO WENGINE
NA
MAJIBU YAKE
Zipo
hoja nyingi ambazo hutolewa na wanaojiita wasabato katika nyakati za leo,
kuhusiana na siku ya Jumapili, lakini zifuatazo ni baadhi tu ya hoja hizo na
majibu yake;
1.
Wasabato hudai kwamba, Wakristo wanaofanya ibada zao siku ya jumapili, ni
makosa mbele za Mungu, maana siyo agizo la Mungu bali ni agizo la mwanadamu.
Hoja
hii si ya msingi na haina ukweli ndani yake. Kwanza kabisa ningependa watu
waelewe kwamba, Wakristo wanaofanya ibada zao siku ya jumapili na siku
nyingine, hao si wanafunzi wa Musa, bali ni wanafunzi wa Bwana wetu Yesu Kristo,
ambaye ndiye mdhamini wa agano lililo bora zaidi, yaani agano jipya, kama
Biblia inavyosema katika Waebrania 7:22,
“Basi kwa kadiri hii Yesu amekuwa
mdhamini wa agano lililo bora zaidi.” Lakini pia, msingi wao, wa kufanya
ibada siku ya Jumapili na siku nyingine, hautokani na torati ya Musa, bali ni
msingi unaotoka kwa Bwana wetu Yesu Kristo (nitaeleza kwa upana katika sura
inayosema ‘Kwa nini Wakristo wanafanya
ibada zao siku ya Jumapili’). Hata hivyo, bado katika agano la kale Mungu
aliagiza watu wakusanyike Jumapili ingawa wasabato wengi hawalioni andiko hilo.
Tukiangalia katika Kutoka 12:16
Biblia inasema, “SIKU YA KWANZA
kutakuwa kwenu na kusanyiko takatifu, na SIKU YA SABA kutakuwa na
kusanyiko takatifu, haitafanywa kazi yoyote katika SIKU HIZO, isipokuwa
kwa hiyo ambayo kila mtu hana budi kula, hiyo tu ifanyike kwenu.” Siku ya
kwanza ya juma ni Jumapili, na siku
ya saba ni Jumamosi kwa kalenda yetu. Kwa hiyo mtoto wa Mungu, mwanafunzi yeyote
wa Musa wa nyakati za leo anapokuja na kukusumbua juu ya siku ya Jumamosi,
mwambie mbona siku ya kwanza ya juma yeye hafanyi ibada na ni agizo la Mungu
kama tulivyokwisha kuona katika Kutoka
12:16.
2.
Wasabato wa leo wanadai kwamba, Wakristo wanafanya kusanyiko siku ya Jumapili,
wana abudu mungu Jua, kwa sababu siku ya Jumapili kwa Kiingereza huitwa
‘Sunday’ ikimaanisha siku ya Jua.
Hoja
hii si ya msingi na haina ukweli ndani yake. Ili tupate kuelewa ukweli wenyewe,
kwanza ni vema tukaziorodhesha siku zote saba kwa kiingereza alafu tuangalie
maana ya siku zote saba, hapo ndipo tutabaini ukweli. Lakini ni vema tukafahamu
kuwa, siku hizi saba, zilipewa majina na wapagani wa Kirumi kulingana na mungu wa
kila siku hiyo, ingawa Mungu alipoumba siku, hakuzipa majina, bali alitumia
siku ya kwanza hadi siku ya saba. Hivyo kuzipa kwao majina ya miungu yao ya
kipagani, haizuii Wakristo wa kweli kumuabudu Mungu wao aliyeumba siku hizo,
maana Yeye ndiye Mzee wa siku. Kwa mfano, siku inapoitwa, siku ya Nyerere
(Nyerere day) ikiangukia Jumamosi, je tutasema wasabato wanamwabudu Mwalimu
nyerere, na hivyo kuwafanya wasifanye ibada siku hiyo? Kwa sababu serikali
imetangaza siku hiyo ni siku ya Nyerere (Nyerere day). Au siku ya ukimwi
duniani, ikiangukia Jumamosi, je itawazuia wasabato wasifanye ibada siku hiyo,
kwani ni siku ya ukimwi, hivyo wakifanya ibada zao watakuwa wanamwabudu mungu
ukimwi? Ebu sasa turudi kwenye kuangalia majina ya siku zote saba kwa
Kiingereza na maana yake;
>Jumatatu
(Monday) - inatokana na moon
day, kwa wapagani wa nyakati zile
ilimaanisha
siku ya kumwabudu mungu moon (mwezi).
>Jumanne
(Tuesday) –inatokana na tiw’s
day, kwa wapagani wa nyakati zile
ilimaanisha ni siku ya mungu Tiw.
>Jumatano
(Wednesday) –inatokana na wedn
day au woden day, kwa wapagani
ilimaanisha siku ya mungu wedn au
woden.
>Alhamisi
(Thursday) –inatokana na thor
day, kwa wapagani ilikuwa ni siku ya
kumwabudu
mungu thor.
>Ijumaa
(Friday) - inatokana na frig
day au freia day, kwa wapagani
ilikuwa ni
siku ya
mungu frig au freia.
>Jumamosi
(Saturday) –inatokana na Saturn
day (siku ya sayari zohari), kwa
wapagani
ilikuwa ni siku ya kumwabudu mungu wa
Kirumi aitwaye
Saturn yaani kwa Kiswahili sayari ya
zohari.
>Jumapili
(Sunday) –ilitokana na sun
day (siku ya jua), kwa wapagani wa
Kirumi
ilikuwa ni siku ya kumwabudu mungu sun
(jua).
Kwa
ujumla, Siku zote za juma, Warumi walizipa majina ya miungu yao, kwa sababu hao
kwa kipindi hicho ndiyo walikuwa watawala. Swali linakuja, kwa vile zimepewa
majina ya miungu ya kipagani, hivyo siku zote hazifai kufanya ibada? Siku ya
Jumamosi, Warumi walikuwa wakimwabudu mungu Saturn kwa Kiswahili zohari, swali
ni kwamba, kwa kufanya ibada zao Jumamosi, wasabato wote wanamwabudu mungu
zohari yaani sayari ya zohari (Saturn)?
Mtoto wa Mungu ni lazima ufahamu kwamba, kupewa jina baya la siku,
halikuzuii wewe siku hiyo kumwabudu Mungu wa kweli, kwa sababu jina hilo
halitoki kwa Mungu bali hutoka kwa mwanamu ambaye hajawahi kuiumba siku. Kwa
hiyo kama msabato atakwambia kuwa unafanya ibada Jumapili (Sunday) hivyo
unamwabudu mungu jua, basi wewe utamjibu unafanya ibada Jumamosi (Saturday),
hivyo unamwabudu mungu sayari ya Saturn (zohari). Hata hivyo wanaomwabudu Mungu wa kweli siku ya Jumapili, hawafanyi
ibada kwa mungu jua, bali wanafanya ibada kwa Mungu wa kweli aliyeumba Jua.
3.
Wasabato hudai kwamba, kwa vile Bwana Yesu aliingia hekaluni siku ya sabato
(Marko 1:21; Luka 4:31), hivyo alishika sabato.
Hoja hii pia si ya msingi na wala
si ya kweli. Katika utafiti wangu nilioufanya, nimegundua kuwa waumini wa
dhehebu la wasabato, asilimia 99 hawaelewi maana ya neno sabato, na hata
walipoletewa dhehebu hili kutoka Marekani, walikuwa hawajatafuta kuchunguza
maandiko kama watu wa Beroya (Matendo
17:11-12). Sabato maana yake ni pumziko la kazi, na kuingia hekaluni haina
mahusino na neno sabato. Kuingia hekaluni siku ya kwanza ya juma (Jumapili) na
siku ya saba kwa wana wa Israeli ilikuwa ni agizo la kusanyiko la kawaida (Kutoka 12:16). Ila kama Biblia ingesema
Bwana Yesu alipumzika kufanya kazi siku ya sabato, hapo tungesema kuwa alishika
sabato.
Anayejua kuwa Bwana Yesu alishika sabato au la ni wasabato halisi
(Mafarisayo) wa nyakati za Yesu, maana hao ndiyo waliopewa kushika sabato na
Mungu mwenyewe, na siyo wanaojiita wasabato leo ambao wameagizwa kushika sabato
na waanzilishi wa dhehebu hilo. Ebu tuwasikilize wasabato halisi (Mafarisayo)
zama za Yesu wanasemaje, je Bwana Yesu alishika sabato au la? Katika kitabu cha
Yohana 9:16 Biblia inasema, “Basi baadhi ya Mafarisayo wakasema, Mtu
huyu hakutoka kwa Mungu, KWA SABABU HASHIKI SABATO. Wengine wakasema,
awezaje mtu mwenye dhambi kufanya ishara kama hizo, kukawa matengano kati yao.”
Unaona ukweli kutoka kwa wasabato halisi, wanakiri kabisa kwamba, Bwana Yesu
hakushika sabato. Bwana Yesu siku ya sabato aliendelea kufanya shughuli zake
kama kawaida, Yohana 5:16-18 Biblia
inasema, “Basi kwa sababu hiyo Wayahudi
walizidi kutaka kumwua, KWA KUWA HAKUIVUNJA SABATO TU, bali pamoja na
hayo, alimwita Mungu Baba yake.” Oh Halleluya! Tunaona jinsi Bwana wetu
alivyovunja sabato na ndiyo maana, wakataka kumwua. Kama kweli, katika Agano
jipya tunashika sabato, mbona Bwana wetu aliivunja sabato, na Yeye ndiyo
kiongozi mkuu wa wokovu wetu (Waebrania
2:10)? Sasa ndugu jiulize, unamfuata Musa au unamfuata Bwana Yesu
aliyeivunja sabato? Kama unamfuata Musa hutafika mbinguni, kwani yeye mwenyewe
alishasema habari za kumfuata Bwana Yesu na siyo yeye, Kumbukumbu 18:15, tunasoma, “Bwana,
Mungu wako, atakuondokeshea nabii miongoni mwa ndugu zake kama nilivyo mimi; msikilize
yeye.” Lakini kama unamfuata Bwana YESU sabato ya nini? Aliivunjwa kwa
kuwa alijua ni kivuli tu, ilikuwa ni ishara yake, sasa yeye aliye pumziko la
kweli amekuja, sasa sabato ya nini? Kama unasema unamfuata Bwana Yesu, na
wakati bado, hautaki kuivunja sabato (kivuli), kamwe hutaweza kuona wokovu
halisi uliotokana na kazi ya msalaba. Kwa kuwa Yeye ndiye kiongozi wako na
Mungu wako, na aliivunja sabato na wewe uivunje, kwa kuwa sisi sote tunamfuata
Kristo kwa kila neno na tendo.
SABABU
ZILIZOPELEKEA BWANA YESU KUINGIA HEKALUNI
SIKU
YA SABATO
Tukisoma
katika kitabu cha Matendo 13:13-15 Biblia
inasema, “Kisha Paulo na wenziwe wakang’oa nanga wakasafiri kutoka pafo, wakafika
Perge katika Pamfilia. Yohana akawaacha akarejea Yerusalemu. Lakini wao
wakatoka Perge, wakapita kati ya nchi, wakafika Antiokia mji wa Pisidia,
wakaingia katika sinagogi siku ya sabato, wakaketi. Kisha baada ya kusomwa
torati na chuo cha manabii, wakuu wa sinagogi wakatuma mtu kwao, na kuwaambia, NDUGU,
KAMA MKIWA NA NENO LA KUWAFAA WATU HAWA, LISEMENI.” Nyakati za Biblia,
kulikuwa na utaratibu kwenye masinagogi kwamba, baada ya kusoma torati na chuo
cha manabii, wakuu wa masinagogi, walikuwa wakikaribisha watu, waliokuwa na
jambo jema la kuwaambia watu kwenye kusanyiko. Sasa, kwa wahubiri kama Bwana
Yesu na Paulo, hii kwao ilikuwa ni nafasi yao ya pekee sana ya kuwahubiria
Wayahudi habari njema za ufalme wa Mungu, kwani walikuwa wamepotea kwa
kuendelea kushika sheria ya sabato na mapokeo mengine. Kwa hiyo, Bwana Yesu na
Mhubiri kama Paulo walitumia nafasi hii, kuwafikishia Mafarisayo na Wayahudi
wengine habari njema, kwa kuwa siku ya sabato, watu wengi walifika hekaluni.
Kwa
hiyo, Bwana Yesu na mitume kama Paulo, hawakwenda hekaluni kukusanyika kwa
kusudi la kushika sabato au kushiriki kusanyiko, bali waliwafuata Wayahudi
waliokuwa bado wamefungwa na mzigo wa sabato na mapokeo mengine. Na kwa
kulithibitisha hilo, Bwana Yesu, alikuwa akienda hekaluni kila siku kufundisha,
na siyo siku ya sabato tu. Luka 19:47
tunasoma, “Naye akawa akifundisha
kila siku hekaluni. Lakini wakuu wa makuhani, na waandishi, na wakuu wa
watu walikuwa wakitafuta njia ya kumwangamiza.” Luka 21:37 tunasoma, “Basi kila
mchana, alikuwa akifundisha hekaluni, na usiku huenda kulala katika mlima
uitwao wa Mizeituni.” Pia katika Yohana 18:20 tunasoma, “Yesu akamjibu, Mimi nimesema na ulimwengu
wazi wazi; siku zote nalifundisha katika sinagogi na katika hekalu, wakusanyikapo
wayahudi wote; wala kwa siri mimi sikusema neno lolote.” Tunaona hapa,
Bwana Yesu, anathibitisha kuwa alikuwa akienda kwenye sinagogi na hekalu kila
siku ili kufundisha watu, kwani ilikuwa ni sehemu ambayo angeweza kuwapata
Wayahudi, hivyo kumpa nafasi ya kufundisha kweli ya neno la Mungu.
4. Hoja ya nne, wasabato hudai kwamba, sheria
ya kushika sabato haijakomeshwa na inaendelea hata sasa kwani imeamriwa kuwa ni
agano la milele kama Biblia inavyosema katika Kutoka 31:16, “Kwa ajili ya hayo
wana wa Israeli wataishika sabato, kuiangalia sana hiyo sabato, katika vizazi
vyao vyote, ni agano la milele.”
Kabla hatujaingia kwa undani zaidi katika kutafuta ukweli wa hoja hii,
ni vizuri, watu wakielewa maana ya neno MILELE kwa msingi wa maisha ya duniani.
Neno MILELE, likitumika kwa matumizi ya kidunia haimaanishi isiyo na mwisho,
kwa kuwa hakuna umilele kwenye maisha ya hapa duniani, bali humaanisha muda
mrefu. Lakini neno MILELE, likitumika nje ya matumizi ya kidunia, mfano maisha
baada ya kufa, hapo ndipo milele humaanisha “isiyo na mwisho”. Kwa ujumla, siyo
kila palipoandikwa kwenye biblia MILELE, inamaanisha isiyo na mwisho. Kwa
mfano, katika kitabu cha 1 Samweli 27:12
tunasoma, “Hivyo akishi akamsadiki
Daudi, akasema, amewachukiza kabisa hao watu wake Israeli; kwa hiyo atakuwa
mtumishi wangu hata milele” Tunaona hapa, Akishi anamtangaza Daudi kuwa
ni mtumishi wake hata milele, lakini, ebu tujiulize, kama kila litumikapo neno
milele, lina maana isiyo na mwisho, je Daudi aliendelea kuwa mtumishi wa
Akishi? Je baadaye hakuwa Mfalme? Akishi hapa, alimaanisha kwamba, Daudi kuwa
mtumishi wake kwa muda mrefu. Mfano mwingine ni pale Bath-sheba alisema, “Mfalme Daudi na aishi milele.” (1 Wafalme 1:31), Bath-sheba alijua kuwa
mwanadamu hawezi kuishi duniani bila kuwa na mwisho, hivyo hapo alimaanisha
Mfalme Daudi aishi kwa muda mrefu. Pia Kumbukumbu
15:17 imezungumzia mtumishi wa milele; hapa haimaanishi mtu anakuwa mtumishi
kwa muda usiyo na mwisho bali kwa muda mrefu.
Mungu alipotumia neno milele kwenye agano la kushika sabato,
hakumaanisha isiyo na mwisho, bali alimaanisha ni agizo la muda mrefu mpaka
wakati wa kuikomesha ulipofika. Na kama, alimaanisha milele ikiwa na maana ya
isiyokoma, je hiyo sabato itashikwa mpaka mbinguni? Na mbinguni hakuna kuhesabu
siku hata tukapata siku ya jumamosi. Pia kama ingekuwa milele ya isiyo koma,
basi kulikuwa hakuna haja ya Bwana Yesu kuja duniani na kuleta agano jipya, na
wala hakukuwa na haja ya Yeye kuwa kinyume na sabato, kama tulivyo kwisha kuona
hapo nyuma. Bwana Yesu ni Mungu, Yeye ndiye aliyeiweka sabato iwe kama kitu cha
kumwakilisha, alipokuwa kabla ya hajakuja duniani. Baada ya kuja alikuwa na
mamlaka ya kuiondoa sawasawa na makusudi yake. Ni sawa tu na tunapotoa
matangazo ya kuja kwa muhubiri fulani au muimbaji fulani, huwa tunaweka picha
yake kwenye vipeperushi na matangazo, lakini muhubiri au muimbaji huyo
akishafika, hatuendelei kuangalia picha zilizo kwenye vipeperushi na matangazo,
bali tunatupa vyote na kwenda kumwona uso kwa uso.
5. Hoja
nyingine kutoka kwa wasabato hujengwa katika kitabu cha Mathayo 5:17-18
inayosema, “Msidhani ya kuwa nalikuja kutangua torati au manabii; la, sikuja
kutangua, BALI KUTIMILIZA. Kwa maana, amini, nawaambia, mpaka mbingu na nchi
zitakapoondoka, yodi moja wala nukta moja ya torati haitaondoka, hata yote
yatimie.”
Hoja
inayojengwa na wasabato katika andiko hili, ni kwamba, Bwana Yesu anakiri
hajakuja kutangua torati wala manabii bali amekuja kuitimiliza, yaani wakimaanisha
kuwa, naye amekuja kuishika sabato. Watoto wa Mungu, hii hoja ni ya
undanganyifu. Kuupata ukweli, ni vizuri turudi kwenye Biblia ya Kiingereza ya
toleo la King James ili tupate tafsiri nzuri zaidi. Mathayo 5:17, “Do not think
that I came to destroy the law or the prophets. I did not come to destroy but
to FULFILL…..” Kadhalika na matoleo mengine ya Kiingereza, neno ‘Kutimiliza’ kwa Kiingereza limetumika ‘FULFILL’. Kulingana na kamusi ya
Kiingereza, neno ‘fulfill’ lina
maana zifuatazo; maana ya kwanza ya ‘fulfill’
ni ‘fill up’ yaani ‘jazia.’ Kwa hiyo inaleta maana ya
kwamba, Bwana Yesu, hakuja kuitangua bali amekuja kuijazia (fill up), kwani kulikuwa kuna mapungufu
katika lile agano. Na ndiyo maana katika kitabu cha Waebrania 8:7 tunasoma, “Maana
kama lile la kwanza, lingalikuwa halina upungufu, nafasi isingalitafutwa kwa
lile la pili.” Maana ya pili ya ‘fulfill’
ni ‘an act of doing something to
satisfaction’ ikiwa na maana kwamba ni kitendo cha kufanya kitu ili kifike
kwenye utoshelevu. Kwa hiyo, Bwana Yesu hakuja kuitangua torati na manabii,
bali amekuja kuboresha ili ifikie utoshelevu, maana bado torati na manabii, haikuleta
utoshelevu wala kuleta matokeo mazuri kwa watu, kwani kila kukicha watu
walikuwa wakiuawa kwa kushindwa kuiishi torati. Maana ya tatu ya ‘fulfill’ ni ‘an act of achieving goal’ kwa Kiswahili inamaanisha ni kitendo cha
kufanya kitu kifike kwenye malengo. Kwa hiyo kwa lugha nyingine tungeweza
kusema kwamba, Bwana Yesu amekuja kuifanya torati na manabii iweze kufikia
malengo aliyokusudia, kwa sababu bado ilikuwa na shida kulingana na uwezo wa
mwanadamu. Sasa kwa lugha fasaha ni kwamba, Bwana Yesu, hakuja kuiondoa torati
na manabii, bali alikuja kufanya maboresho,
marekebisho, masahihisho; ikiwa na
maana kwamba kilichotakiwa kuondoka kiliondoka, na kilichotakiwa kubaki,
kilibaki; na hii ilifanya na chekecho la msalaba. Mfano, mambo ya kushika
sabato yaliondolewa, kwa sababu sabato ilikuwa ni amri ya ishara, ilikuwa ni
kivuli, ikimuashira Yeye Bwana Yesu mwenyewe kama pumziko la kweli la kiroho.
Hivyo, kwa vile Yeye pumziko halisi amekuja, sabato haikuwa na kazi tena. Bwana
Yesu anasema, “Njooni kwangu, ninyi
nyote msumbukao, na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.”(Mathayo 11:28)
Upungufu wa Agano la lake unaozungumziwa katika Waebrania 8:7, haupo katika torati, kwani torati kwa asili, haina
tatizo na ni njema maana ni maagizo ya Mungu mwenyewe. Tatizo lilikuwa kwenye
uwezo wa wanadamu wenyewe katika kuifuata torati yote kwa nguvu zao; maana
kipindi cha agano la kale, walipewa sheria na hukumu tu, lakini hawakuwa na
neema ya kuwafanya washike hiyo sheria. Kwa hiyo, kimsingi wana wa Israeli
waliipenda torati (sheria) na hukumu walizopewa na Mungu, na waliikubali hiyo
torati (sheria) na hukumu, na ndiyo maana walikubali kufanya agano na Mungu,
kwa kuwa kila agano ni lazima kuwepo kwa makubaliano katika pande mbili.
Mioyoni mwao waliikubali na kuipenda torati (sheria) na hukumu zake,
lakini mwili uliwazuia kuitekeleza hiyo torati, kwa kuwa walipewa torati
(sheria) na hukumu tu bila neema au kiwezesho cha kuiishi sheria. Sasa hapo
ndipo tunapopata upungufu wa Agano la kale. Katika kitabu cha Warumi 7:14-16 tunasoma, “Kwa maana twajua kuwa torati asili yake ni
ya rohoni; bali mimi ni mtu wa mwilini, nimeuzwa chini ya dhambi. Maana sijui
nifanyalo; kwa sababu lile nilipendalo, silitendi; bali lile nilichukialo ndilo
ninalolitenda.Lakini kama
nikilitenda lile nisilolipenda, naikiri ile sheria ya kuwa ni njema. Basi sasa
si mimi nafsi yangu ninayetenda hilo, bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu.
Kwa maana najua ya kuwa ndani yangu, yaani, ndani ya mwili wangu, halikai neno
jema; kwa kuwa kutaka nataka, bali kutenda lililo jema sipati.” Kama
nilivyo kwisha kusema hapo nyuma kwamba, wana wa Israeli waliipenda torati na
hukumu. Lakini katika viungo vya mwili yaani utu wa nje, sheria ilikuwa ni kama
ni mzigo mzito sana; kwa sababu kwa asili, ndani ya mtu halikai neno jema. Na
kwa sababu hiyo, wana wa Israeli hawakuweza kudumu katika Agano la kale kama
maandiko yanavyotuambia katika, Waebrania
8:9, “Halitakuwa kama agano lile
nililoagana na baba zao, katika siku ile nilipowashika mikono yao niwatoe
katika nchi ya Misri. KWA SABABU HAWAKUDUMU KATIKA AGANO LANGU, mimi nami
sikuwajali, asema Bwana.” Pia katika kitabu cha Ezekieli 20:21 Biblia inasema, “Lakini watoto hao waliniasi; hawakuenda katika amri zangu, wala
hawakuzishika hukumu zangu kuzitenda, ambazo mwanadamu ataishi kwazo kama
akizitenda; walizitia unajisi sabato zangu; ndipo nikasema, kwamba nitamwaga
ghadhabu yangu juu yao, ili kuitimiza hasira yangu juu yao jangwani.”
Kwa ujumla ukisoma vitabu vyote vya Musa, utagundua kwamba wana wa
Israeli hawakukaa vizuri kwenye sheria na hukumu za lile agano. Ndipo Mungu kwa
huruma yake akaleta Agano lingine, lililo bora zaidi kuliko lile la kwanza, na
mdhamini wa Agano hili ni Mungu mwenyewe, wakati Mdhamini wa agano la kale
alikuwa mwanadmu (Musa). Waebrania 7:22
tunasoma, “Basi kwa kadiri hii Yesu
amekuwa mdhamini wa agano lililo bora zaidi.”
Hivyo basi, ni neno la kuaminiwa, tena lastahili kukubalika, kuwa mweka
sheria katika Agano la kale, amekuja kurekebisha sheria na kufanya Agano upya,
hivyo lile la kwanza kutotenda kazi; Waebrania
8:13 tunasoma, “Kwa kule kusema, Agano
jipya, amelifanya lile la kwanza kuwa kuukuu. Lakini kitu kianzacho kuwa
kikuukuu na kuchakaa ki karibu na kutoweka.”
6.
Katika hoja ya sita, baadhi ya wasabato hudai kwamba hakuna kuokoka duniani na
wala hakuna watakatifu, na wanasimamia hoja hiyo katika maandiko yafuatayo; Mhubiri 7:20; Warumi 3: 12, 23; Warumi
5:12; Zaburi 14:3.
Kabla hatujaingia kwa undani zaidi, si vibaya kama tutafahamu maana ya
neno kuokoka kama linavyotumiwa na watoto wa Mungu. Kuokoka maana yake ni kusalimika kutoka katika hatari iliyo
dhahiri. Kwa mfano, mtu aliyesalimika kufa kwenye ajali ya gari, mtu huyo
tunasema ameokoka na ajali ya gari. Kuokoka
katika dhana ya Kiroho, haina tofauti sana na maana tuliyoizungumzia hapo
nyuma, lakini utofauti wake upo kwenye aina ya hatari. Mtu ambaye hajamwamini
na kumkiri Bwana Yesu, ni wazi kabisa yupo katika hatari ya kwenda kwenye
hukumu ya mateso ya moto wa milele, kama maandiko yanavyotuambia katika Yohana 3:18; Yohana 5:22. Lakini kwa
mtu ambaye amemwamini Mwana wa Mungu, huyo haukumiwi, kwa maana hiyo, mtu huyo anakuwa
ameokoka au amesalimika na hatari ya kwenda kwenye mateso ya moto wa milele; Yohana 3:18 tunasoma, “Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini
amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu.”
Marko 16:16 Maandiko yanasema, “Aaminiye na kubatizwa ATAOKOKA; asiyeamini
atahukumiwa.” Waefeso 2:5
Maandiko yanakiri kwamba tumeokolewa kwa neema. Kadhalika maandiko katika Isaya 45:20 tunasoma, “Jikusanyeni mje; na kukaribia pamoja, ninyi
wa MATAIFA MLIOOKOKA…..”
Jambo la msingi ambalo watu wanapaswa kufahamu ni kwamba, baba yetu
Adamu alipofanya dhambi, na sisi wanadamu wote, tukahesabiwa kuwa tuna dhambi
kama maandiko yanavyosema katika Warumi
5:12. Kwa hiyo, kama kwa kuasi kwake baba yetu Adamu, na sisi sote
tukaingizwa katika hali ya wenye dhambi, basi kwa kutii kwake mmoja ambaye
Bwana wetu Yesu Kristo, na sisi tunaomwamini tumeingizwa katika hali ya wenye
haki yaani utakatifu (Warumi 5:19). Adamu
alipokosea na sisi tukawa tumekosea, Bwana Yesu alipopatia na sisi tukawa
tumepatia. Kwa hiyo ni dhahiri kabisa kuokoka ni hapa duniani, na wakamilifu
wapo duniani, na Zaburi 16:3
maandiko yanasema, “Watakatifu waliopo
duniani ndiyo walio bora, hao ndio niliopendezwa nao.” Paulo anawaita wenzake watakatifu, 2 Wakorintho 13:13 tunasoma, “Watakatifu wote wawasalimu.” Paulo pia anathibitisha kuwepo kwa watakatifu
duniani katika Wafilipi 4:21-22
tunasoma, “Msalimieni kila MTAKATIFU
katika Kristo Yesu. Ndugu walio pamoja nami wawasalimu. WATAKATIFU wote
wawasalimu, hasa wao walio wa nyumbani mwa Kaisari.”
Mungu mwenyewe anamthibitisha Ayubu kuwa alikuwa
mkamilifu (Ayubu 1:8). Maandiko
yanatuthibitishia kuwa Nuhu pia alikuwa mtu wa haki na mkamilifu (Mwanzo 6:9). Watoto wa Mungu, ukamilifu
tunaupata hapa hapa duniani na siyo mbinguni, na ndiyo maana Bwana Yesu anasema
katika Mathayo 5:48, “Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba
yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.” (Soma pia Waebrania 12:14, Walawi
19:2).
KUSHIKA
SIKU YA SABATO KUNAAMBANA NA TORATI YOTE YA MUSA
Maandiko, katika kitabu cha Yohana
1:17 yanasema, “Kwa kuwa torati
ilitolewa kwa mkono wa Musa; neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo.”
Watoto wa Mungu, ni jambo la msingi sana kufahamu kwamba, tunapotaja neno torati, tunamaanisha Amri kumi, sheria 613 na hukumu zake.
TORATI
= AMRI KUMI + SHERIA 613 + HUKUMU ZAKE
Kwa
nyakati za agano la kale, ilikuwa, huwezi kuwa mkamilifu kwa kushika amri kumi
tu bila kushika na sheria nyingine 613 na kuzitendea kazi hukumu zake. Mtu
asiyetendea kazi yote yaliyoandikwa katika torati, alikuwa amelaaniwa; Galatia 3:10 tunasoma, “Kwa maana wale wote walio wa matendo ya
sheria, wako chini ya laana; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu asiyedumu
katika YOTE yaliyoandikwa katika kitabu cha torati, ayafanye.” Mungu aliwaagiza wana wa Israeli washike
torati yote; Walawi 20:22 tunasoma,
“Basi zishikeni amri zangu ZOTE, na
hukumu zangu zote, na kuzifanya; ili kwamba hiyo nchi, ambayo nawapeleka ninyi
kuiketi isiwatapike.” Pia Kitabu cha
Kutoka 35:10 Biblia inasema, “Na kila mtu kati yenu aliye na moyo wa
hekima na aje, na kuyafanya haya YOTE ambayo Bwana ameagiza.” Kwa mtu
anayeng’ang’ania sheria ya kushika sabato na makatazo ya baadhi ya vyakula katika
nyakati hizi za Agano jipya, mtu huyo ni wazi kabisa, hayupo kwenye fungamano
la Agano Jipya, maana tumeona bayana kwamba, sheria hii, Bwana hakuipitisha,
kwa kuwa ilikuwa ni ishara, iliyokuwa ikimuashiria Yeye kama (sabato) pumziko
la kweli la kiroho (Wakolosai 2:16-17).
Hivyo kushika sabato ni kukataa sheria ya Kristo na kuikubali sheria ya Musa.
Na sharti la sheria ya Musa (torati) ni kwamba, ni lazima mtu ashike Amri kumi
zote, sheria nyingine 613 na hukumu zake. Mfano; sheria ya kushika sabato
ilikuwa na hukumu yake, pale ambapo mtu, alionekana kutoitimiza, yaani alipaswa
kuuawa; Kutoka 31:14 tunasoma, “Basi mtaishika hiyo sabato; kwa kuwa ni
takatifu kwenu; kila mtu atakayeitia unajisi hakika yake atauawa, kwa kuwa kila
mtu afanyaye kazi katika siku hiyo, nafsi hiyo itakatiliwa mbali na watu wake.”
Kitabu cha Kutoka 35:2 Biblia
inasema, “Fanyeni kazi siku sita, lakini
siku ya saba itakuwa siku takatifu kwenu; ni sabato ya kustarehe kabisa kwa
Bwana; mtu awaye yote atakayefanya kazi yoyote katika siku hiyo ATAUAWA.”
Kama
Mungu alitoa agizo la kushika sabato, na pia akatoa agizo kuwa atakayefanya
kazi yoyote siku hiyo ni lazima auawe; Je ni wasabato wangapi leo tunawaona
wanafanya kazi Jumamosi, kama kuna usahihi wowote mbona hatuoni wakiitekeleza
hukumu ya kuuana? maana ni agizo la Mungu mwenyewe. Yakobo 2:10 inasema mtu akiishika sheria yote, akajikwaa katika
neno moja tu, amekosa juu ya yote. Wapendwa! hii ndiyo sababu iliyompelekea
Bwana Yesu kuivunja sabato, baadhi ya sheria na hukumu zote; kwa kuwa ilikuwa
ni huduma ya mauti (2 Wakorintho 3:7).
Mtu anayeshika sheria ya sabato katika nyakati hizi za agano jipya, anapaswa
kushika na amri tisa zote, pamoja na sheria 613 na hukumu zake, ambazo zote
zimefafanuliwa kwenye vitabu vya Kutoka, Mambo ya Walawi, Hesabu na Kumbukumbu
la torati. Lakini kama Wayahudi walishindwa, sisi tutaweza wapi? Watoto wa
Mungu, tusikubali kujitwisha mizigo ambayo Bwana wetu alikwisha itua, kwa nini
tuendelee kukaa kwenye makosa yaliyofanyika katika agano la kwanza; Waebrania 9:15 tunasoma, “Kwa sababu hii ni mjumbe wa agano jipya,ili,
mauti ikiisha kufanyika, KWA KUKOMBOA MAKOSA YALIYOKUWA CHINI YA AGANO LA
KWANZA, hao walioitwa waipokee ahadi ya urithi wa milele.” Kazi ya torati
(ikiwemo sheria ya sabato) ilikuwa ni kama kiongozi cha kutuleta kwa Bwana Yesu
kama maandiko yanavyosema katika kitabu cha Wagalatia 3:24-26 tunasoma, “Hivyo
torati imekuwa kiongozi kutuleta kwa Kristo, ili tuhesabiwe haki kwa imani.
Lakini, iwapo imani imekuja, hatumo tena chini ya kiongozi (torati-ikiwemo
sabato).” Sabato ni kama kiongozi cha kutuleta kwa Kristo maana Yeye ndiye
sabato mwenyewe (pumziko), sasa kwa vile Kristo amekuja, sasa hatupasWi
kuing’ang’anisa sabato.
MADHARA
YA KUSHIKA SHERIA YA SABATO
1. Kushika sabato kuna mfanya mtu asiwe mwana
funzi wa Yesu, bali mwanafunzi wa Musa, kwa kuwa torati ilikuja kwa mkono
wa Musa na neema na kweli vilitolewa kwa mkono wa Yesu (Yohana 1:17).
2. Kushika siku ya sabato ni mafundisho
manyonge na yenye upungufu, hivyo kumfanya mtu awe mwana wa Jehanamu mara
mbili (Mathayo 23:15). Kitabu cha Wagalatia 4:9-10 Biblia inasema, “Bali sasa mkiisha kumjua Mungu, au zaidi
kujulikana na Mungu, kwa nini kuyarejea tena mafundisho ya kwanza yaliyo
manyonge, yenye upungufu, ambayo mnataka kuyatumikia tena? MNASHIKA SIKU, na
miezi, na nyakati, na miaka.”
3. Kushika sabato, kunamfanya mtu kuwa chini
ya laana. Na hii ni kwa sababu sabato ni sheria iliyo katika torati; na
tunaposema torati, tunamaanisha amri kumi, sheria 613 na hukumu zake. Na
ilikwisha kuandikwa kuwa mtu asiyeshika torati yote ni amelaaniwa; Galatia 3:10 tunasoma, “Kwa maana wale wote walio wa matendo ya
sheria, wako chini ya laana; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu asiyedumu
katika YOTE yaliyoandikwa katika kitabu cha torati, ayafanye.” Kristo ndiye aliyetukomboa kutoka katika
laana ya torati (Wagalatia 3:13), na
ndiyo maana ukimwamini Bwana YESU, ni lazima ufuate sheria ya Kristo (Wagalatia 6:2), na siyo sheria ya Musa.
Kushika sabato (pumziko) siyo sheria ya Kristo, na Bwana Yesu na Baba yake
waliipinga kama tunavyoweza kusoma katika Yohana
5:16-18, “Kwa sababu hiyo Wayahudi
wakamwuudhi Yesu, kwa kuwa alitenda hayo siku ya sabato. AKAWAJIBU, BABA YANGU
ANATENDA KAZI HATA SASA, NAMI NINATENDA KAZI. Basi kwa sababu hiyo
Wayahudi walizidi kutaka kumwua, kwa kuwa HAKUIVUNJA SABATO TU, bali
pamoja na hayo, alimwita Mungu Baba yake, akijifanya sawa na Mungu.” Swali
ni hili, huyu Yesu liyeshika sabato na kuwafundisha watu leo washike sabato ni
Yesu yupi?
3. Kushika sabato kuna mfanya mtu awe mwilini;
na mtu anayeufuata mwili ni ngumu sana kumpendeza Mungu (Warumi 8:8), kwa kuwa hatoweza kushinda dhambi. Na ndiyo maana
utaona mtu anashika sabato, lakini bado haogopi kwenda kwa waganga wa kienyeji,
haoni ni makosa kubishana, haoni dhambi kufanya uasherati na uzinzi. Kwake
kuinadi sabato ndiyo injili, kuliko kumnadi Bwana Yesu.
4. Kushika sabato kunatengeneza ngome ya
kifarisayo ndani ya mtu; na madhara ya ngome hii ni kwamba, hata kama mtu
akisikia ukweli kutoka kwa Mungu mwenyewe, bado mtu huyo hawezi kuusikia wala
kuufuata ukweli huo. Ufahamu wa mtu unafungwa hata nuru ya wokovu isimzukie (2 Wakorintho 4:4), hivyo moja kwa moja
mtu anakuwa amekata tiketi ya kwenda Jehanam ya moto.
5. Kushika sabato kunamfanya mtu awe mnafiki.
Mtu mnafiki huwa na kawaida ya kutangaza sheria na kuitilia mkazo, lakini yeye
mwenyewe haitendei kazi. Luka 13:15
Biblia inasema, “Lakini Bwana akamjibu
akasema, Enyi wanafiki, kila mmoja wenu, je! Hamfungui ng’ombe wake au punda
wake siku ya sabato katika zizi, aende naye kumnywesha?” Na ukweli ni kwamba hakuna mnafiki
atakayeurithi ufalme wa Mungu.
KUKOMESHWA KWA SABATO
Agizo
la kushika siku ya sabato na torati yote kwa ujumla, ilikuwa ni huduma ya mauti
au huduma ya adhabu ya kifo; Katika kitabu cha 2 Wakorintho 3:7-8 tunasoma, “Basi,
ikiwa huduma ya mauti iliyoandikwa na kuchorwa katika mawe, ilikuja katika
utukufu, hata Waisraeli hawakuweza kuukazia macho uso wa Musa, kwa sababu ya
utukufu wa uso wake; nao ni utukufu uliokuwa ukibatilika. Je huduma ya roho
haitazidi kuwa katika utukufu?” Kwa hiyo torati yote ikiwemo kushika
sabato, ilikuwa ni huduma ya mauti. Pia torati haikuwa huduma ya mauti tu, bali
ilikuwa ni nguvu za dhambi, kama maandiko yanavyosema katika kitabu cha 1 Wakorintho 15:56, “Uchungu wa mauti ni dhambi, na nguvu za
dhambi ni torati.” Kwa kadiri unavyozidi kuifuata torati ndivyo nguvu ya
dhambi inavyozidi, kwa kuwa torati kazi yake ni kubaini makosa. Haina tofauti
na darubini ya kupima vijidudu vya magonjwa. Kwa vile torati ilikwisha tolewa
katika agano la kale na imetufanya kujua dhambi nini; hivyo katika agano jipya,
haupaswi tena kuifuata torati, bali tunapaswa kuifuata dawa ya dhambi, ambayo
ni Bwana wetu Yesu Kristu. Warumi 8:2 Biblia inasema, “Kwa sababu sheria ya Roho ya uzima ule ulio katika Kristo Yesu
imeniacha huru, mbali na sheria ya dhambi na mauti.”
Kwa
ujumla ni kwamba, torati ilikuwa ni huduma ya mauti, kwa kuwa sheria
walizoshindwa kuzifuata Wana wa Israeli, iliwalazimu kuuawa. Watu wengi
walikufa kwa nguvu ya torati; mfano mtu ambaye hakushika sabato aliuawa (Kutoka 31:14-15; Kutoka 35:2-3). Mtu
aliye jaribu kukusanya kuni siku ya sabato kwa kusudi la kujipikia chakula
aliuawa (Hesabu 15:32-36). Watu
wagonjwa hawakutakiwa kutibiwa siku ya sabato hivyo kusababisha watu wengi kufa
(Luka 13:14), kitu ambacho si mpango
wa Mungu.
Hata hivyo, pamoja na torati kuwa ni huduma
ya mauti, pia Wana wa Israeli wenyewe, hawakuweza kudumu katika lile agano la
kwanza walilofanya na Mungu, hivyo kufanya agano hilo, kutofanikiwa; Yohana 7:19 tunasoma, “Je! Musa hakuwapa torati? Wala hakuna mmoja
wenu aitendaye torati.” Ni vema ifahamike kuwa, kinachofanya agano kudumu,
ni kutimizwa kwa masharti au sheria au taratibu za agano husika. Katika agano
lolote au mkataba wowote ule, ni lazima kuwepo kwa masharti au sheria
zilizowekwa, ili kuulinda mkataba au agano hilo. Kwa hiyo mtu anayevunja sheria
katika mkataba au agano fulani, tayari yeye, ndiye anayekuwa amevunja huo
mkataba au hilo agano. Wana wa Israeli walifanya agano na Mungu, na agano hilo
lililindwa na vifungu vya sheria ambavyo ni torati yote; sasa kwa vile wote
walikosa kuitendea kazi torati kama tunavyoona katika Yohana 7:19; Ezekieli 20:21, hivyo, kitendo cha kutoitendea kazi
torati, tayari walikwisha vunja agano la kwanza na siyo Mungu. Na ndiyo maana
zama za Nabii Isaya, Bwana alimtumia Nabii huyo kuwaambia wana wa Israeli
kwamba yeye hataki tena sabato zao na ibada zao; Isaya 1:13 tunasoma, “Msilete
tena matoleo ya ubatili; uvumba ni chukizo kwangu; mwezi mpya na SABATO, kuita
makutano; siyawezi maovu hayo na makutano ya ibada.”
Vitu hivi vyote, havikuwa na maana tena
mbele za Mungu kwa kuwa tayari wana wa Israeli walikwisha liharibu Agano Lake.
Na kama agano lilikwisha haribika, kushika sabato na ibada zao zilikuwa na
maana gani mbele za Mungu? Hivyo kwa huruma yake, aliamua kufanya mpango mpya
wa kuweka agano jipya na sheria zikiwa zimeboreshwa.
Kabla ya kukomeshwa kwa sabato na agano la
kwanza kwa ujumla, Mungu kwa hekima yake alianza kuwatumia manabii kutoa
matangazo juu ya ujio wa agano jipya na kukomeshwa sabato;
1.
Nabii Hosea alitoa unabii juu ya kukomeshwa kwa
sabato na siku za kusanyiko zilizoamriwa. Hosea
2:11 tunasoma, “Tena nitaikomesha
furaha yake yote, na sikukuu zake, na siku zake za mwandamo wa mwezi, NA
SABATO ZAKE, na makusanyiko yake yote yalioamriwa.”
2.
Baada ya kutofanikiwa kwa torati, Musa alitangaza
kabisa ujio wa mdhamini wa agano jipya (Bwana Yesu) na ujio wa sheria ya
Kristo. (Kumbukumbu 18:15-19).
3.
Nabii Isaya alianza kupiga debe juu ya ujio wa
agano jipya (Isaya 55:3).
4.
Yeremia naye hakubaki nyuma, naye alianza kupiga
mbiu juu ya agano jipya (Yeremia 31:31;
32:40).
SABABU
ZA NYONGEZA ZA KUKOMESHWA KWA SABATO NA TORATI YOTE KWA UJUMLA
1.
Torati ilikuwa ni kivuli tu cha mema yatakayo
kuja na haikuwa kitu halisi. Waebrania
10:1 tunasoma, “Basi torati, kwa
kuwa ni kivuli cha mema yatakayokuja, wala si sura yenyewe ya mambo hayo,
kwa dhabihu zile zile wanazozitoa kila mwaka daima, haiwezi wakati wowote
kuwakamilisha wakaribiao.” Sabato ni sehemu ya torati, hivyo wanaoshika
sabato, ni vema waelewe kuwa, sabato si kitu halisi, ilikuwa ni kivuli tu.
2.
Torati ni kiongozi tu cha kutuleta kwa Yesu. Wagalatia 3:24-26 tunasoma, “Hivyo torati imekuwa kiongozi kutuleta kwa
Kristo, ili tuhesabiwe haki kwa imani. Lakini iwapo imani imekuja, hatupo tena
chini ya kiongozi.” Mfano; Wewe ni mgeni, na umefika maeneo ambayo unataka
kukutana na mwenyeji wako, na wakati huo huo, ukakutana na mtu usiyemjua, na
kwa baati nzuri huyo mtu, akasema kuwa mwenyeji wako unayemtafuta, ninafahamu
alipo, hivyo, akaamua kukupeleka. Baaada ya huyo mtu kukufikisha, je utaamua
kumng’ang’ania huyo aliyekupeleka au utabaki na mwenyeji wako, uliyekusudia
kufika kwake. Sasa sabato ilikuwa ni kiongozi cha kutupeleka kwa Kristo, sasa
kwa sababu tumempata Kristo, hatuhitaji tena sabato.
3.
Torati ilikuwa haiondoi uhitaji yaani ilikuwa
haitibu dhambi bali ilikuwa ikibaini dhambi na kuadhibu. 2 Wakorintho 3:15-16 tunasoma, “Ila hata leo, torati ya Musa isomwapo, utaji huikalia mioyo yao. Lakini
wakati wowote watakapomgeukia Bwana, ule utaji huondolewa.”
4.
Kuwa chini ya torati ni kuwa chini ya laana, kwa
sababu ilimlazimu mtu kuifuata torati yote bila kuacha hata kitu kimoja. Hii
haikuwezekana, hivyo kuwafanya watu wote kuwa chini ya laana (Wagalatia 3:10; 5:3-4).
5.
Torati huchochea nguvu ya dhambi (1 Wakorintho 15:56).
ANGALIZO
1.
Torati (ikiwemo na sheria ya kushika sabato) pamoja
na manabii, vilikuwapo mpaka Yohana mbatizaji; Luka 16:16 Biblia inasema, “Torati
na manabii vilikuwapo mpaka Yohana; tangu wakati huo habari njema ya ufalme
wa Mungu, hutangazwa, na kila mtu hujiingiza kwa nguvu.” Kwa hiyo, kushika
sabato ilikuwa mwisho wake nyakati za Yohana Mbatizaji na siyo nyakati hizi za
Agano jipya.
2.
Watu waliompokea Bwana Yesu kuwa Bwana na
mwokozi wa maisha yao, hao ni wahudumu wa Agano jipya; 2 Wakorintho 3:6, tunasoma, “Naye
ndiye aliyetutosheleza, kuwa wahudumu wa Agano jipya; si wa andiko, bali wa
Roho, kwa maana andiko huua, bali Roho huhuisha.”
3.
Katika nyakati hizi za Agano jipya, hatuifuati
torati bali tunaifuata sheria ya Kristo (Wagalatia
6:2). Wagalatia 5:14 tunasoma, “Maana torati yote imetimilika katika neno
moja, nalo ni hili, umpende jirani yako kama nafsi yako.” Kitabu cha Mathayo 22:37-40 tunasoma, “Akamwambia, mpende Bwana Mungu wako, kwa
moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote. Hii ndiyo amri
iliyo kuu, tena ni ya kwanza. Na ya pili yafanana nayo, nayo ni hii, mpende
jirani yako kama nafsi yako. Katika amri hizi, hutegemea torati yote na manabii.”
Hizi zote ni miongoni mwa sheria ya Kristo; Wagalatia 6:2 inasema, “Mchukuliane
mizigo na kuitimizwa hivyo sheria ya Kristo.”
4.
Bwana YESU alifanya kazi siku ya sabato (Yohana 5:16-18; Yohana 9:16), lakini
bado Biblia inasema hakufanya dhambi (Waebrania
4:15). Kushika sabato nyakati za leo ni maagizo ya waanzilishi wa dhehebu
hilo na siyo maagizo ya Bwana YESU (Waanzilishi
hao ni William Miller 1782-1849; Hiram Edson; Joseph Bates na Hellen Gould
White).
5.
Mpendwa mtoto wa Mungu, kushika sabato katika
Agano jipya si maagizo ya Mungu, kamwe usikubali kuifuata, maana utatolewa kutoka
katika uanafunzi wa Yesu na kuwa mwanafunzi wa Musa. Na isitoshe neno la Mungu
katika Wakolosai 2:16 linasema, “Mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au
vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au SABATO. Mambo hayo
ni kivuli cha mambo yajayo; bali mwili ni wa Kristo.” Mtu akikwambia kuhusu
kushika sabato au sheria za kutokula vyakula na kunywa vinywaji, mwambie, “Siwezi kushika kivuli, maana Biblia inasema
hayo yote yalikuwa ni kivuli cha mambo yajayo, bali ninamshika Kristo.”
6.
Anayeitegemea torati (ikiwemo na sabato), huyo
ni kiongozi kipofu, mkufunzi wa wajinga na mwalimu wa watoto wachanga. Warumi 2:17-20 tunasoma, “Lakini wewe ukiwa unaitwa Myahudi na
kuitegemea torati, na kujisifu katika Mungu, na kuyajua mapenzi yake, na
kuyakubali mambo yaliyo bora, nawe umeelimishwa katika torati, na kujua hakika
ya kuwa wewe mweyewe u kiongozi wa vipofu, mwanga wao walio gizani, mkufunzi wa
wajinga, mwalimu wa watoto wachanga, mwenye namna ya maarifa na ya kweli katika
torati.”
SABABU ZINAZOWAPELEKEA WAKRISTO KUFANYA
JUMAPLI KUWA SIKU YAO YA KUSANYIKO KUU LA IBADA.
Kwa kipindi kirefu kumekuwapo na migogoro kwa
Wakristo kuhusu siku halali ya kufanya ibada. Wakristo wanaoshika sheria ya
siku ya sabato wamekuwa wakidai kuwa siku halali ya kufanya ibada ni Jumamosi,
kadhalika na Wakristo wanaofanya ibada zao siku ya Jumapili husema kuwa siku
halali ya kufanya ibada ni siku ya Jumapili. Kama majadiliano haya yangefanywa
kwa msingi wa kimaadiko, basi nina amini kabisa kwamba, kamwe kusingekuwa na
mgogolo wowote, kwa kuwa Neno la Mungu liko wazi kabisa. Ni vema ifahamike
kwamba, Mungu wetu anapenda sana kuona watoto wake wakimwadudu kila siku na
kila saa, na wala siyo katika siku fulani au masaa fulani. Matendo 26:7 Biblia inasema, “Ambayo
kabila zenu kumi na mbili wanataraji kuifikia, wakimwabudu Mungu kwa bidii
mchana na usiku……”
Lakini kwa vile sisi ni wanadamu, na
tunahitaji kufanya shughuli za kutupatia mkate wa kila siku, hatuwezi kufanya
kusanyiko la kumwabudu Mungu kila saa, hivyo hatuna budi kuwa na siku maalumu
za makusanyiko. Bwana Yesu, kupitia Mutme Paulo amefundisha wazi wazi kuhusu
siku za kufanya makusanyiko; Warumi
14:5-6, Biblia inasema, “Mtu mmoja
afanya tofauti kati ya siku na siku, mwingine aona siku zote kuwa sawasawa. Kila
mtu na athibitke katika akili zake mwenyewe. Yeye aadhimishaye siku,
huiadhimisha kwa Bwana; naye alaye hula kwa Bwana…….” Swala la siku ipi
watu wafanye kusanyiko, lipo chini ya maamuzi ya watu husika, kwa kuwa siku
zote ni sawa, wanaweza wakachagua siku fulani na wakawa wanafanya makusanyiko,
kwa kuwa kila aadhimishaye siku huiadhimisha kwa Bwana. Kama watu wataamua
kufanya makusanyiko kila siku bado ni jambo jema.
Utaratibu wa kufanya makusanyiko ya ibada
siku ya Jumapili haukuanzishwa na Mfalme Constantine kama wanavyodai baadhi ya
watu. Kabla ya Mfalme Constantine, Mitume katika kanisa la kwanza walikuwa
wakikusanyika siku ya Jumapili; 1
Wakorintho 16:1-2 tunasoma, “Kwa
habari ya ile changizo kwa ajili ya watakatifu, kama vile nilivyoamuru makanisa
ya Galatia, nanyi fanyeni vivyo. Siku ya kwanza ya juma kila mtu kwenu
na aweke akiba kwake; kwa kadiri ya kufanikiwa kwake; ili kwamba michango
isifanyike hapo nitakapo kuja.” Pia Matendo
20:7-12 tunasoma, “Hata siku ya
kwanza ya juma, tulipokuwa tumekutana kuumega mkate…..” Kwa hiyo,
watoto wa Mungu wanaweza wakamwabudu Mungu katika siku zote saba, kwani Mungu
hatazami siku, bali anawatafuta waabuduo halisi, ambao wanamwabudu Baba katika
Roho na pia katika Kweli (Yohana 4:23-24).
SABABU ZA MSINGI ZINAZOWAPELEKEA WAKRISTO
KUFANYA JUMAPILI KUWA SIKU YAO KUU YA KUSANYIKO LA IBADA
1.
Mungu alikwisha iweka katika Agano la kale siku ya Jumapili kama siku ya
kusanyiko ikiwa kama kiashirio cha siku ya matumaini kwa Wafuasi wa Kristo,
kwani siku hii ndiyo Bwana alifufuka; Kutoka
12:16 tunasoma, “Siku ya kwanza
kwenu kutakuwa na kusanyiko takatifu, na siku ya saba kutakuwa na kusanyiko
takatifu…” Kwa hiyo agizo la kukusanyika siku ya Jumapili lilianza tangu
Agano la kale kama kiashirio na kuthibitika katika Agano jipya.
2.
Jumapili ni sikukuu ya malimbuko au mazao ya kwanza ambayo ilifanywa katika
Agano la Kale, siku ya pili baada ya sabato (on the morrow after the Sabbath) (Walawi 23:9-14), ambayo ilifanywa kama
kivuli cha sikukuu ya kufufuka kwa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye ndiye limbuko
lao waliolala mauti, mzaliwa wa kwanza katika wafu (1 Wakorintho 15:20; Wakolosai 1:18).
3.
Jumapili ni siku ya ushindi wa Bwana wetu Yesu Kristo dhidi ya kifo na mauti.
Alifufuka siku hiyo na kujidhihirisha kwa wanafunzi wake. Wokovu wetu
unahusiana moja kwa moja na kufufuka kwa Yesu Kristo. Kufa na kufufuka ndiko
kunakomtofautisha Bwana Yesu na manabii wengine. Yohana 20:1 tunasoma, “Hata
siku ya kwanza ya juma Mariam Magdalene alikwenda kaburini alfajili,
kungali giza bado; akaliona lile jiwe limeondolewa kaburini.” Baada ya kufufuka siku ya kwanza ya juma
ambayo ndiyo Jumapili, Bwana Yesu alikuwa akiwatokea wanafunzi wake siku ya
kwanza ya juma, kuashiria kuwa hiyo ni siku ya matumaini wa wanafunzi wa Yesu (Yohana 1:19, 26). Kwa wanafunzi wa
Yesu, siku ya Jumamosi haikuwa siku ya matumaini kwa kuwa siku hiyo bado Bwana
alikuwa kaburini, na shetani na malaika zake bado walikuwa wakitamba siku hiyo.
Kwa hiyo Jumapili ina maana kubwa sana kiroho kwa wanafunzi halisi wa Yesu.
4.
Jumapili ndiyo siku aliyokuja duniani kiongozi mkuu wa kazi yote ya Mungu
katika Kanisa yaani ROHO MTAKATIFU. Na huyu ndiye Bwana wa mavuno anayewapeleka
watenda kazi shambani mwa Bwana. Roho Mtakatifu alikuja sawa sawa na ahadi ya
Kristo, siku ya pentekoste ambayo ni Jumapili, siku inayofuata baada ya sabato
(Matendo 2:1). Roho Mtakatifu
alichagua kuja Jumapili ili kuanzisha siku mpya ya matumaini ya kumwabudu Mungu
katika Roho na Kweli (Yohana 4:23-24).
5. Siku
ya Pentekoste yaani Jumapili, ndiyo siku ya kwanza ambayo kanisa la kwanza la
Mitume lilianza mahubiri kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, na watu 3,000 wakaokoka
na kubatizwa na kuanza kusanyiko la kwanza la ibada kanisani (Matendo 2:1-41). Torati ilipotambulishwa
ilisababisha kuuawa kwa watu wengi sana, lakini neema na kweli ilipotambulishwa
ilisababisha kuokolewa kwa watu wengi sana.
6.
Wakristo wa Kanisa la kwanza la Mitume walikusanyika katika ibada siku ya
kwanza ya juma yaani Jumapili (1Wakorintho
16:1-2). Mtume Paulo alifundisha katika ibada iliyofanyika siku ya kwanza
ya Juma yaani Jumapili (Matendo 20:7-12).
Neno linatuagiza kumfuata Paulo kama yeye anavyomfuata Kristo (1 Wakorintho 11:1), hivyo na sisi
hatuna budi kufanya kusanyiko siku ya Jumapili. Pia ni muhimu kufahamu kuwa
kanisa limejengwa chini ya msingi wa Mitume na Manabii na Kristo akiwa jiwe kuu
la pembeni. Hivyo walichofanya Mitume na Manabii wa Yesu ndivyo nasi tunapaswa
kufuata.
Lakini hata hivyo Wakristo halisi tunapaswa
kujifunza Neno la Mungu na kumwomba Mungu kila siku na siyo Jumapili tu. Mitume
walidumu ndani ya hekalu kila siku; (Matendo
2:46) tunasoma, “Na siku zote
kwa moyo mmoja walidumu ndani ya hekalu, wakimega mkate nyumba kwa nyumba….”
MAREKEBISHO
YA SHERIA KATIKA AGANO JIPYA
KUPITIA
CHEKECHO LA MSALABA
Mungu habadiliki katika tabia na sifa zake,
lakini Yeye mwenyewe amekuwa akiweka amri na kuzibadili kama apendavyo Yeye,
katika vizazi mbalimbali. Na pia amekuwa akifanya maagano na vizazi mbalimbali
kwa kadiri ya kusudi lake.
Adamu na Hawa hawakupewa torati, bali
walipewa amri moja tu, yaani kutokula matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya
kama Biblia inavyosema katika kitabu cha Mwanzo
2:16-17. Mungu hakumpa Adamu amri ya ‘usizini’
kwa kuwa hakuwapo mwanamke mwingine ila mkewe Hawa. Vivyo hivyo hakumpa amri ya
‘usiibe’ kwa kuwa vitu vyote vilivyo
kuwapo katika bustani ya edeni alipewa na Mungu kuwa vyake. Pia Mungu
asingeweza kumwambia Adamu aheshimu wazazi wake kwa kuwa hawakuwapo. Katika
maandiko hatuoni Mungu akimwagiza Adamu ashike sabato. Kwa hiyo zama za Adamu
na Hawa walipewa amri moja tu.
Tukija zama za Nuhu, tunaona Nuhu naye
anafanya agano na Mungu na kupewa sheria zifuatazo katika Mwanzo 9:1-7; sheria ya kwanza Nuhu anaambiwa asile nyama pamoja na
uhai wake yaani damu (Mwanzo 9:4-5),
na sheria ya pili, Nuhu na kizazi chake wanakatazwa kuua (Mwanzo 9:6).
Tukija kwa Ibrahimu tunaona Mungu anafanya
agano na Ibrahimu na kumwambia awe mkamilifu (Mwanzo 17:1). Lakini pia anampa sheria mpya ya kutahiri nyama ya
magovi yao, kitu ambacho Nuhu hakuamriwa kufanya.
Baada
ya kuja uzao wa Yakobo yaani wana wa Israeli, tunaona wanapewa torati na hukumu
kupitia Musa. Hivyo basi, Mungu amekuwa akitoa amri na kuzibadili kizazi hadi
kizazi. Kubadilika kwa sheria kulingana na nyakati si kitu kigeni, hayo ni
mapenzi yake na hakuna mwanadamu wa kuhoji. Kazi yetu wanadamu kama
watekelezaji wa amri za Mungu, ni kuwa na akili na kufahamu nyakati tulizo nazo,
na amri zipi tunapaswa kuzitenda katika nyakati hizi tulizo nazo. Maadiko
katika kitabu cha 1 Nyakati 12:32
yanasema, “Na wana wa Isakari, watu
wenye akili za kujua nyakati, kuyajua yawapasayo Israeli wayatende; vichwa
vyao walikuwa watu mia mbili na ndugu zao wote walikuwa chini ya amri yao.”
Siyo kwa sababu Ibrahimu aliambiwa na Mungu kutahiri mtoto wa kiume wa siku
nane, na sisi katika Agano jipya tufanye hivyo, la hasha.
Leo sisi hatumo katika maongozi ya Agano la
kale likiongozwa na torati, bali tumo katika maongozi ya Agano jipya
tukiongozwa na sheria ya Kristo (Wagalatia
6:2) na siyo na torati ya Musa.
MAREKEBISHO
YA SHERIA KATIKA AGANO JIPYA
Marekebisho ya sheria katika Agano jipya,
inajumuisha vitu vifuatavyo; kwanza, kupitishwa kwa baadhi ya sheria kutoka
katika Agano la kale kama zilivyo; pili, kupitishwa kwa sheria za Agano la kale
baada ya kufanyiwa maboresho; tatu, kutopitishwa kabisa kwa baadhi ya sheria za
Agano la kale, sheria hizo ni kama kushika sabato, makatazo ya baadhi ya
vyakula pamoja na kuondolewa kwa hukumu; na nne, kuwekwa kwa sheria mpya.
Katika kutopitishwa kabisa kwa baadhi ya
sheria katika Agano la kale, Bwana Yesu, aliziondoa sheria ambazo zilikuwa ni kivuli
yaani zilizoashiria kitu fulani kijacho, mfano sabato (pumziko) ilikuwa ni
kivuli au ishara iliyomwashiria kuja kwa Bwana Yesu ambaye ndiye pumziko
halisi, ni kwa sababu hiyo basi, kushika sabato katika Agano jipya kuliondolewa
na chekecho la msalaba, kwa kuwa sheria hii ilimwakilisha Bwana Yesu mwenyewe
kama pumziko halisi (sabato). Hivyo kwa vile pumziko (sabato) mwenyewe amekuja,
haina haja ya kuendelea kushika kivuli au ishara.
Pia
kuna sheria za Agano la kale ambazo zimepita katika Agano jipya lakini baada ya
Bwana Yesu, kuzifanyia marekebisho kwa kuziboresha, yaani kuziweka kiroho zaidi.
Kwa ujumla sheria kuu katika torati, ambazo ziligoma kupita kwenye chekecho la
msalaba ni Kushika sabato, sheria ya makatazo ya vyakula na hukumu za torati. Kuhusu sabato, Bwana
Yesu hakushika sabato na wala hakuwaruhusu wanafunzi wake kushika sabato kama
tulivyokwisha kuona hapo nyuma kwa upana sana(Marko 2:23-28; Yohana 9:16; Yohana 5:16-18); Pia katika torati
walikatazwa kula baadhi ya vyakula yaani wanyama n.k, lakini katika Agano
jipya, Bwana Yesu aliwaagiza mitume wake wale chochote watakachowekewa mbele
yao, tena wale bila kuuliza, maandiko yafuatayo yanatupa mwongozo wa kula
vyakula vyote (Luka 10:8; Marko 7:18-20;
Mathayo 15:11; Tito 1:15; Wakolosai 2:16; 1 Timotheo 4:3-5; Warumi 14:14, 20;
Matendo 11:6-9); Kadhalika kuhusu hukumu walizopewa wana wa Israeli nyakati
za Musa, Bwana Yesu alipokuja, aliziondoa kwa kusema, “Msihukumu msije mkahukumiwa.” (Mathayo
7:1-2; Luka 6:37).
Katika Mathayo 5:21-43 tunaona Bwana Yesu akifanya marekebisho ya sheria kwa uwazi
kabisa tena mbele za watu, Mathayo
5:21-22 “Mmesikia watu wa kale
walivyowaambia, Usiue…..Bali mimi nawaambieni…..” Bwana Yesu hapa anairekebisha
sheria kwa kuiboresha. Mathayo 5:27-28,
“Mmesikia kwamba imenenwa, Usizini,
lakini mimi nawaambia kila amtazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini
naye moyoni…” Mathayo 5:31-32, “Imenenwa pia, mtu akimwacha mkewe, na ampe
hati ya talaka; lakini mimi nawaambia kila mtu amwachaya mkewe……..” Kwa
ujumla ukisoma Mathayo 5:21-43 yote
utaona jinsi Bwana alivyofanya marekebisho ya sheria.
KUHANI
MPYA NA SHERIA MPYA
Moja ya utofauti kati ya Agano la kale na
Agano jipya ni ukuhani. Katika Agano la kale Kuhani alikuwa ni mwanadamu ambaye
ni Haruni na uzao wake (mdhambi). Lakini katika Agano jipya kuhani ni Mungu
mwenyewe yaani Yesu Kristo (Mkamilifu).Na maandiko katika kitabu cha Waebrania 7:12 yanasema, “Maana ukuhani ule ukibadilika, hapana budi
sheria nayo ibadilike” Kuhani wa
Agano la kale alikuwa ni kuhani wa sheria ya amri iliyo ya jinsi ya mwili,
lakini kuhani wa Agano jipya ambaye ni Yesu Kristo, Yeye ni kuhani wa sheria ya
nguvu za uzima usio na ukomo kama Neno la Mungu linavyosema katika Waebrania 7:16, “Asiyekuwa kuhani kwa sheria ya amri iliyo ya jinsi ya mwili, bali kwa
nguvu za uzima usio na ukomo.” Kwa hiyo ni dhahiri kabisa, kwamba kwa kuwa
kuhani amebadilika na sheria nayo katika Agano jipya imebadilika.
ANGALIZO
KWA WANAOSHIKA SHERIA YA SABATO
Kushika sabato, makatazo ya vyakula au
vinywaji na hukumu, ni miongoni mwa amri katika torati ya Musa. Na amri hizi,
Bwana Yesu, hakuzipitisha katika Agano la jipya kama tulivyokwisha kuona katika
sura zilizopita. Kwa hiyo, amri hizo, si miongoni mwa sheria za Kristo (Wagalatia 6:2). Kimsingi, unapofundisha
au kuishika torati ya Musa, unawapofusha watu wasione kazi ya msalaba, hivyo
watu hao watajiita wakristo, lakini ni watu wenye tabia za mwilini. Kadhalika
unapofundisha na kuyashika maagizo ambayo yapo kinyume na mmiliki wa mbingu,
ambaye ni Bwana Yesu Kristo, ni wazi kabisa huko ni kujiweka au kuwaweka watu karibu
na shimo la jehanamu ya moto.
Kwa kawaida mtu anayeisogelea torati ya Musa
(kushika sabato, makatazo ya vyakula na vinywaji), hutafuta tamaa za dhambi na
hatimaye mtu huyo huzalia mauti; Warumi
7:5 tunasoma, “Kwa maana tulipokuwa
katika hali ya mwili, tamaa za dhambi, zilizokuwapo kwa sababu ya torati,
zilitenda kazi katika viungo vyetu hata tukaizalia mauti mazao.”
Lakini pia, mtu anayeshika torati ya Musa
katika nyakati hizi za Agano jipya yaani kushika sabato na makatazo ya vyakula
au vinywaji n.k, mtu huyo huitwa mwanafunzi wa Musa na wala si mwanafunzi wa
Yesu, kwa kuwa torati ilikuja kwa mkono wa Musa na neema na kweli kwa mkono wa
Kristo (Yohana 1:17). Hata kama mtu
anamtaja Bwana Yesu, na mtu huyo akawa anashika sheria za Musa yaani kushika
sabato makatazo ya vyakula au vinywaji n.k, bado mtu huyo ataendelea kutafunwa
na nguvu ya torati. Na zifuatazo ni dalili za mtu anayemtaja Yesu lakini bado
nguvu ya torati inamtafuna;
1.
Mtu huyu huwa na tabia ya unafiki (nje huonekana
ni mtakatifu lakini rohoni ni mdhambi)-Mathayo
6:2; Mathayo 23:25-28. Mafarisayo walikuwa na tabia hii, hivyo na mtu
anayeshika torati atakuwa na tabia hii.
2.
Mtu huyu huwa na tabia ya kupenda kubishana, kwa
kuwa torati inamfanya asiwe rohoni. Hushawishika kwa hekima yenye kushawishi
akili na si kwa dalili za roho na nguvu (1
Wakorintho 2:4-5).
3.
Mtu huyu huwa na tabia ya kujihesabia haki,
wakati wote hujiona sahihi, wakati amepotea, nguvu ya torati humpofusha asione
ukweli (Mathayo 7:1-2).
4.
Mtu wa namna hii, huwa na tabia ya kuinadi
sheria moja ambayo anaimudu kuishika, mfano, anaweza kuwa mtu huyo anashika
sana sheria ya sabato, basi atainadi hiyo sabato kuliko kumnadi Kristo. Hata
kama atamwona mtu anafanya uasherati, ili mradi anashika sabato, huyo kwake ni
mtakatifu.
5.
Mtu wa namna hii huwa na tabia ya kuwaudhi walio
zaliwa kwa roho yaani waliookoka; Wagalatia
4:29 tunasoma, “Lakini kama vile
siku zile yule aliyezaliwa kwa mwili alivyomwudhi yule aliyezaliwa kwa Roho,
NDIVYO ILIVYO NA SASA.”
6.
Mtu huyu huwa na juhudi ya kumtumikia Mungu
lakini si katika Roho na kweli, hivyo huwafanya waongofu wawe wana wa jehanamu
mara mbili (Mathayo 23:15).
7.
Mtu wa namna hii huwa na wema wa kujionesha
mbele za watu na si wema halisi (Mathayo
6:1).
8.
Ni ngumu mtu wa namna hii kushinda dhambi, kwa
sababu ya nguvu ya torati inayomkalia kutenda dhambi.
Ukifanya uchunguzi wa kina, utagundua kuwa,
waanzilishi wa dhehebu la wanaoshika sabato, hawakuwa wanatheolojia na watu
waliojua maandiko; na wala hawakukaa chini ya mafundisho ya wachungaji wao.
Mwanzilishi wa Kwanza ni Mmarekani aitwaye William Miller, alizaliwa
Pittsfield, Massachusetts, mwaka 1782 na kufariki mwaka 1849. Mtu huyu aliacha
ukristo, lakini baadaye aliamua kurudi tena kwenye ukristo mwaka 1816, na ndiye
aliyeleta mafunuo ya uongo ya kurudi kwa Bwana Yesu mwaka 1844, hata
kusababisha hasara na mtafaruku mkubwa sana miongoni mwa wafuasi wake (Wana
majilio-Adventists). Mwanzilishi wa pili ni Hiram Edson, huyu alikuwa ni mfuasi
wa Miller, na ndiye aliyechangia mafundisho potofu ya hukumu ya upelelezi
kwenye dhehebu hilo, baada ya unabii wao wa kurudi kwa Yesu kutotimia. Mwanzilishi
wa tatu ni aliyekuwa baharia zamani, mtu aitwaye John Bates, huyu bwana ndiye
aliyetoa mchango mkubwa wa kurudisha sabato ya Agano la kale. Na ndiye wa kwanza kutoa mafundisho ya uongo
kwamba, Jumapili ni alama ya mnyama, bali siku ya sabato ndiyo muhuri wa Mungu
kwa watu wake walio waaminifu. Mwanzilishi wanne ni Bwana James na mke wake
aitwaye Ellen Gould White, hawa ndiyo waliouendeleza usabato kuliko mtu
mwingine yeyote. James na mkewe walijiunga na Miller mwaka 1840 na 1842 na hii
iliwapelekea kutengwa na kanisa lao la Methodist. Ellen ndiye aliyekuja kuyakazia
mafundisho ya kushika sabato, baada ya kudai kuwa alipelekwa mbinguni na kukuta
katika amri kumi za Mungu amri ya nne ya kushika sabato, ilikuwa iking’aa
kuliko zote.
Kimsingi, hawa wote hawakuwa watu walioijua
Biblia bali walienda kwa nguvu ya upeo mdogo wa kimaandiko waliokuwa nao. Kubwa
zaidi ni nguvu ya pesa katika kueneza mafundisho, na hata kufanya kusambaa
sehemu kubwa hususani Afrika.
Watoto wa Mungu, ni lazima tutambue kuwa
sisi sote tumeokolewa kwa neema, na wala si kwa matendo ya sheria (Waefeso 2:8-9). Kama tutaishi kwa
kufuata mambo ya mwili, hapo tunataka kufa, bali kama tutayafisha matendo ya
mwili kwa roho, hapo tutaishi, kwa kuwa wanaongozwa na Roho, hao ndiyo wana wa
Mungu (Warumi 8:13-14).
Godwin Gunewe